UCHAGUZI WA
WANACHAMA WA TFF
Kamati ya
Uchaguzi ya TFF katika kikao chake kilichofanyika Septemba 15, 2012 ilijadili
michakato ya uchaguzi wa vyama wanachama wa TFF inayoendelea hivi sasa kabla ya
kufanyika Uchaguzi Mkuu wa TFF mwishoni mwa mwaka huu. Kamati iliamua
yafuatayo;
Chama cha
Mpira wa Miguu Mkoa wa Njombe (NJOREFA)
Kamati ya
Uchaguzi ya TFF ilibaini kuwa uongozi wa muda wa NJOREFA haukutoa ushirikiano wa
kutosha kuiwezesha Kamati ya Uchaguzi ya NJOREFA kuanza mchakato wa uchaguzi kwa
tarehe kwa tarehe iliyokuwa imepangwa na hivyo kusababisha kuchelewa kuanza kwa
mchakato huo wa uchaguzi wa mkoa huo mpya.
Kamati
imebaini pia kuwa kutokana na changamoto za kiuongozi zinazoukabili mkoa huo
mpya, mchakato wa uchaguzi ulioanza Septemba 2, 2012 haukuzingatia kikamilifu
Kanuni za Uchaguzi za Wanachama wa TFF.
Kutokana na
kasoro hizo za msingi, mchakato wa uchaguzi wa NJOREFA utaanza upya Septemba 18,
2012 ukizingatia Kanuni za Uchaguzi za Wanachama wa TFF. Uchaguzi wa NJOREFA
utafanyika Oktoba 28, 2012.
Chama cha
Mpira wa Miguu Mkoa wa Tabora (TAREFA)
Kamati
ilibaini kuwa kuna mkanganyiko katika mchakato wa uchaguzi wa TAREFA na kwamba
mkanganyiko uliotokea umesababishwa na Kamati ya Uchaguzi ya TAREFA kutotimiza
wajibu wake wa kusimamia uchaguzi wa TAREFA kwa mujibu wa Kanuni za Uchaguzi za
Wanachama wa TFF.
Kutokana na
kuvurugika kwa mchakato wa uchaguzi wa TAREFA uliosababishwa na kiwango kikubwa
cha ukiukwaji wa Kanuni za Uchaguzi, Kamati ya Uchaguzi ya TFF imejiridhisha
kuwa Kamati ya Uchaguzi ya TAREFA haina uwezo wa kusimamia majukumu ya uchaguzi
wa TAREFA na kuzingatia kikamilifu matakwa ya Kanuni za Uchaguzi ya Wanachama wa
TFF.
Kwa kuwa
Kamati ya Uchaguzi wa TAREFA imeshindwa kutimiza wajibu wake na hivyo
kusababisha mkanganyiko na uvurugaji wa uchaguzi wa TAREFA, Kamati ya Uchaguzi
ya TFF kwa mamlaka yake yaliyoainishwa katika Katiba ya TFF Ibara ya 49(1) na
Kanuni za Uchaguzi za Wanachama wa TFF Ibara ya 10(6), 26(2) na (3) imeamua
yafuatayo;
(i)
Imefuta Kamati
ya Uchaguzi ya TAREFA. Uongozi wa TAREFA unatakiwa kuteua Kamati mpya ya
Uchaguzi itakayoandaa na kutekeleza majukumu yake ikizingatia Kanuni za Uchaguzi
za Wanachama wa TFF na Katiba ya TAREFA. Uteuzi wa Kamati mpya ya Uchaguzi ya
TAREFA ufanyike kabla ya Septemba 24, 2012.
(ii)
Imefuta
mchakato wa uchaguzi wa TAREFA. Mchakato wa uchaguzi utaanza upya Septemba 25,
2012 na uchaguzi utafanyika Novemba 4, 2012.
Vyama vya
Mpira wa Miguu mikoa ya Manyara (MARFA) na Kilimanjaro
(KRFA)
Uchaguzi wa
MARFA na KRFA utafanyika Septemba 22, 2012 kama
ilivyopangwa.
UTENDAJI WA
KAMATI ZA UCHAGUZI ZA WANACHAMA WA TFF
Kamati
imebaini baadhi ya viongozi wa vyama vya wanachama wa TFF wanaomaliza muda wao
wanashiriki kudhoofisha michakato ya uchaguzi ya vyama vya mpira wa miguu kwa
kutotoa fursa kwa Kamati za Uchaguzi za vyama wanachama kuanza michakato ya
uchaguzi kwa tarehe zilizopangwa na Kamati ya Uchaguzi ya
TFF.
Kwa kuwa ni
wajibu wa viongozi waliopo madarakani kuhakikisha kuwa vyama vyao vinafanya
uchaguzi kwa mujibu wa Katiba zao na Kanuni za Uchaguzi, Kamati ya Uchaguzi ya
TFF haitasita kupendekeza kwa Mamlaka husika za TFF vyama hivyo kuchukuliwa
hatua za Kikatiba kwa kushindwa kutimiza matakwa ya Katiba ya TFF kwa kuwa na
uongozi ambao muda wa ukomo wa madaraka utakuwa umepita na hivyo kutokidhi
matakwa ya Ibara ya 12(2)(a) ya Katiba ya TFF.
Kamati ya
Uchaguzi ya TFF inavishauri vyama wanachama wa TFF kuzingatia ratiba ya uchaguzi
na Kanuni za Uchaguzi za Wanachama wa TFF wakati wote wa michakato ya uchaguzi
wa viongozi wa vyama vyao. Viongozi walioko madarakani wanatakiwa kutoa
ushirikiano kwa Kamati za Uchaguzi kama ilivyoianishwa kwenye Kanuni za
Uchaguzi.
Hamidu
Mbwezeleni
Makamu
Mwenyekiti kamati ya uchaguzi